> English
Katika insha hii, nilitumia maoni ya watoto juu ya hatua dhidi ya adhabu ya upigaji bakora iliyotekelezwa katika skuli kumi za majaribio kwenye muktadha wa mradi wa ulinzi wa mtoto ulioendeshwa na jumuiya ya Save the Children pamoja na serikali ya Zanzibar. ‘Sanduku la maoni’ liliwekwa katika yale skuli kumi za majaribio mwanzo wa mradi kwa ajili ya kukusanya maoni ya watoto. Nilisoma na kutathmini maoni wa watoto 1,342 kwa ujumla katika skuli saba za mradi majaribio yaliyokusanyiwa katika kipindi cha miaka miwili 2012 hadi 2014. Kusudio la kukusanya maoni ni kuwezesha kujenga ufahamu kuhusu mtazamo wa watoto katika mradi wa ulinzi wa mtoto uliolenga kupiga marufuku utumiaji wa bakora maskulini katika kuwaadabisha watoto na kujenga hali ya usalama maskulini.
Maoni yalionyesha kwamba ingawa baadhi ya walimu waliacha kuwapiga watoto bakora, walimu wengine walianza kutumia yaliyoangaliwa kama ‘adabu mbadala/nidhamu endelevu’ kwa mfano kuwadai watoto walipe pesa au walete vifaa vya skuli. Maoni yalionyesha kwamba wengi wa watoto walikataa kuendelea kupigwa kama aina ya nidhamu. Hata hivyo, wengine pia walikataa kutokupigwa. Ninafahamu ukatazaji kwa maelezo ya Audra Simpson kama ‘dalili, mazoea, uwezekano wa kufanya mambo kwa njia tofauti’ (2017: 29). Ninapendekeza kwamba ukatazaji huu wakati huo huo wa kupigwa na kutopigwa (kwa majadiliano ya undani angalia Fay 2021, sura ya 4) ni zaidi ya kusema ‘hapana’ kwa mwelekeo wa adhabu ya bakora au aina mbadala wa nidhamu iliyotekelezwa na jumuiya ya kimataifa ya ulinzi wa mtoto iliyolenga kuibadilisha. Ukatazaji wa watoto wa aina mbili yanaonyesha changamoto watoto wanayoipata pale njia ya nidhamu mbadala inadhalisha udhalimu kama ule ambao tayari wanayajua.
Ikiwa ukatazaji ni ‘chaguo kwa kuzalisha na kudumisha miundo mbadala ya mawazo, siasa na mila na desturi mbali na pia katika uhusiano wa kihakiki na taifa’ (Simpson 2017: 19) inabidi maoni tofauti ya ukatazaji wa watoto (kukubali kupigwa na kutokubali kupigwa) yanajenga maswala katika imani na vitendo vikubwa vya ulinzi wa mtoto. Kwa njia ya kukubali na kukataa adhabu ya bakora, maoni haya ya watoto kizanzibari yanayopingana na kupigwa au kuadabishwa kwa aina nyingine yanaonyesha kuna umuhimu wa jumuiya ya ulinzi wa mtoto – ya kizanzibari na ya kimataifa – kufikiria upya utawala wa haki za watoto maskulini ibadilishwe vipi. Ufahamu wa muda wa utotoni kama nafasi ya kiukweli na muhimu utotoni kwa ajili ya upingaji wa kihakiki utawezeshwa tu kwa njia ya utumiaji ya nadharia na uwakilishi kitaalamu (Spyrou, Rosen, & Cook, 2019: 6), tukiwasikiliza ukatazaji wa watoto kwa undani zaidi.
Wakati mwanzo watoto walikubali kutopigwa na kuadabishwa kwa njia nyengine, mwisho walikataa kwamba njia nyengine za kuadabishwa ni ‘bora’ kuliko kupigwa. Msemo wa ‘kushika ukweli’ (Simpson 2017: 26) kwamba vitendo vya kulipa pesa au kununua mafagio kama vyombo vya skuli – viliangaliwa kama ‘mbadala’ au ‘adabu mbadala/nidhamu endelevu’ katika skuli za majaribio – siyo afadhali kuliko kuvumilia kupigwa bakora mara mbili tatu katika mazingira ambayo maisha ya watoto wengi na familia zao yanaathiriwa na umaskini.
Hivyo, badala ya kulaumu upigaji bakora wanafunzi wengi walipendelea iendelezwe au irudiwe, iwezekanavyo kwa sababu ya mtihani mgumu watoto waliyofanyiwa na njia mbadala yaliyotekelezwa. Wanafunzi (angalia maoni 1 chini) ambao hawakuikataa bakora walisema kwamba bakora ziendelee kwa ajili ya wanafunzi wajisikie wana nidhamu na adabu nzuri, utii, heshima, tabia njema, na kutochelewa. Wanafunzi waliokataa bakora kuendelea (angalia maoni 2 chini) walisema hivyo kwa sababu ya maradhi, maumivu, majeruhi, kupendelea urafiki kuliko ukali, na hali ya kuendelea kupigwa licha ya mradi wa adabu mbadala kuanzishwa tayari. Mwisho, wanafunzi (angalia maoni 3 chini) waliokataa aina tofauti ya adabu/adhabu mbadala walieleza kwamba ukatazaji dhidi ya kulazimika kulipa pesa au kuletea vifaa vya skuli kama mafagio kama njia mbadala ya kupigwa, kulazimishwa kuwaingiza wazazi wao katika suluhisho za adabu zao maskulini, na kuambiwa na wazazi wao kudai kupigwa tena kuliko kulazimishwa kulipa pesa.
Badala ya kukubali kiukweli kwamba kupigwa bakora kwa ajili ya adabu ni bora, ukatazaji ya aina mbili ya watoto inasisitiza ukosefu wa uchaguzi katika muktadha ya mfumo wa ulinzi wa mtoto inayotarajia kuwahudumia lakini ambayo bado haijakuwa decolonised kwa njia ya kuwazingatia mahitaji tofauti ya watoto na vipaumbele vyao badala ya kuwa sawa duniani na kuiweka peke yake matarajio ya haki za watoto tu. Kupinga kwa watoto dhidi ya miundo iliyoletwa yanaonyesha, kwa kiwango kikubwa, udhalimu wa miundo na usambazaji wa nguvu ambayo siyo sawa katika uzoefu wa watoto wa upigaji wa bakora lakini pia katika miradi iliyowekwa kupinga huo upigaji. Wakati wanaharakati wa haki za watoto wanakubali kwamba watoto wasipigwe maskulini, watoto wenyewe wanaweza kukubali kuwa njia mbadala inayotekelezwa kuchukua nafasi ya kupiga bado hazijakaa sawa.
Kwa kuchukua kwa uzito kupinga kwa watoto – na pia panaposhangaza – njia zote mbili upigaji bakora na ulinzi wa mtoto, mbinu kujitoa katika ukoloni katika utaalamu wa utotoni na anthroplojia (Cheney 2018, 2020; Fay 2019) yanafahamu ukatazaji kwa maana mbili ya ‘unyeti wa utafiti na msimamo wa kisiasa’ (Rosen 2021) inaweza kusaidia kupinga ufahamu mdogo kuhusu ulinzi wa mtoto unaoweza kuwawekea watoto katika mazingira hatari nyengine. Ikiwa kama wanaantropolojia na wataalamu wa masomo ya utotoni ‘tungetumia kitendo cha ethnography yenyewe kama ukatazaji’ (Simpson 2017: 29) – kumaanisha tufahamu ushiriki wa ethnography kikamilifu kuhusu mambo ulinzi wa mtoto ambayo mara nyingi inaangaliwa kama kutohitaji kuhojiwa – tungeweza kufaulu kuchangia kupanua eneo la shirika la watoto kutoa uhakiki na kupinga miundo ya nguvu ambayo wanakabiliwa nayo katika jamii yao na watendaji wale wanaoingilia kwao.
Maoni 1: “Bakora ziendelee”: Kuidhinisha adhabu ya bakora
The cane should continue. Maoni yangu tuendelee kupigwa bakora kwa sababu ukiangalia wanafunzi wanachelewa, hawaandiki na tatizo la utoro. Ahsante. Bakora ziendelee kwa kila anayefanya kosa na mwenye kwenda kinyume cha kanuni za skuli na sheria za skuli. Tukipi[g]wa tutasikia tutafahamu na tutakuwa wakarimu. Bora tupigwe kwa sababu: a) tutakuwa tunachelewa, b) tutakuwa hatuaniki, c) tutakuwa hatuwaheshimu walimu wetu, d) tutakuwa mwalimu akututuma hatuendi, e) tutakuwa hatuna adabu na pia tutafanya mambo yasiyokubalika shule n.k. Maoni yangu ni tuendelee kupigwa bakora kwa sababu wanafunzi hawana nidhamu kama vile kuchelewa kuja skuli, kufanya mazogo madarasani na kutoandika kazi. Viboko viendelee pale mtu/mwanafunzi atakapofanya kosa. Ahsante. Bora tupi[g]wa makwaju: kwani tusipopi[g]wa makwaju tutachelewa, hatutoandika na tutakuwa hatuna adabu. Asante.
Maoni 2: “Sitaki kupigwa mimi naumwa”: Kukataa adhabu ya bakora
(…) tunaomba mikwaju ipunguzwe kwa walimu wote kwani wengine ni wagonjwa na tunaomba msipinge kichwani Ahsante walimu wote. Tunaomba skuli yetu isiwe na bakora. Maoni yangu kuwa ilianzishwa adhabu mbadala, adhabu mbadala hiyo kua wanafunzi tusipigwe mbona leo hii tunapigwa. Kwa iyo tusipigwe wanafunzi. Sitaki kupigwa mimi naumwa. Wanafunzi wasipigwe kwa sababu wakipigwa wanaumizwa vipi adhabu mbadala ipo au haip[o]. (…) skuli iwe na mazingira mazuri kila mwanafunzi awe na kumpyuta skuli iwe ya horofa na iwe na mafeni (…) na mikwaju ipunguzwe wakiwemo walimu wakutosha. Ashanteni. Bakora zisiendele ila kwa walokuwa wakorofi wanastahili adhabu ambayo itakayowafanya wajikeribishe kwa makosa ambayo wanayafanya. Ninaomba kila darasa liwe na feni japo moja. Skuli yetu ipakwe rangi vizuri. Walimu wapunguza kupiga. Walimu waongezeke. Wawe wanasomesha kwa bidii. Ili wanafunzi wapate kufaulu.
Maoni 3: “Tunachukuliwa pesa zetu tunazopewa na wazazi wetu”: Kukataa malipo kama adhabu mbadala
Mazumuni ya barua hii tunakujulisheni kwamba walimu hawatupi azabu uliyokusudia wanatutoleshea pesa kila siku hii ni azabu mbadala. Adabu mbadala si kutoleshwa pesa. Wazee wetu wanasema bora tupigwa bakora kuliko kutoa mafagio kwa sababu tunawapa shida wazee wetu. Walimu wanasomesha vizuri tena vizuri sana lakini wanafunzi nao wakaidi sana. Na wanaokaa mbali wasitoleshwe pesa wala fyagio. Hii si skuli ya kweli. Tunachukuliwa pesa zetu tunazopewa na wazazi wetu. Madhumuni ya barua hii kukujulisheni kwamba walimu wanatutolesha pesa zetu kila siku hii adabu au malipo. Asanteni sana. Tuachieni tupumue na pesa zetu za tabu. Iondolewe adhabu mbadala kwa sababu inatuumiza sisi wengine tunakaa mbali. (…) na pia kuondosha adhabu ya mafyagio kwa sababau wazee wetu hawana pesa na pia sisi ni wanafunzi tunategemea wazee wetu. Na pia kupunguza kupiga kwani ukali sio kufahamisha bali mwalimu awe ana urafiki na mwanafunzi kwa sababu akawa ana urafiki na mwanafunzi ataweza kufahamishwa kwa urahisi na pia (…) darasa lina mashimo kama gerezani tunaomba tujengwe darasa. Ahsante. Na ninaomba tunapochelewa tusichangishe mifyagio bora tupigwa mikwaju kuliko kuchangisha mifyagio kwani siku hizi mafyagio bei hali.
Cite as: Franziska Fay, “Ukatazaji wa Watoto na Ulinzi wa Mtoto,” in Reimagining Childhood Studies, 23rd June 2021, https://reimaginingchildhoodstudies.com/childrens-refusal-child-protection-swahili/